find more job local and international,We are here to help you get job you want at a right time, make sure you subscribe to our blog as a member in order to send you a current job,
Saturday, 1 October 2011
NEC KUTANGAZA MATOKEO NDANI YA SAA 24
PRESHA imezidi kupanda Igunga. Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ikiahidi kutangaza matokeo ya ubunge katika jimbo hilo ndani ya saa 24, vyama vitatu vikubwa CCM, Chadema na CUF vimeendelea kushutumiana kila kimoja kikidai kuhujumiwa.Usiku wa kuamkia jana, CCM kikiwatumia walinzi wake wa Green Guard kiliwazingira vijana 120 wa Chadema kwa tuhuma za kuingia na silaha ili kuvuruga uchaguzi huo uliopangwa kufanyika kesho.
Wakati Chadema kwa upande wake kikidai kwamba kitendo hicho cha CCM ni kiwewe cha kushindwa uchaguzi huo, CUF kimekuja na tuhuma nzito dhidi ya Nec kwamba inakiandalia ushindi chama tawala, CCM.
Madai ya CCM
Viongozi wa CCM wakiongozwa na Katibu wa Idara ya Siasa na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sekretarieti ya Halmashauri ya CCM, January Makamba waliwavamia vijana hao wa Chadema waliokuwa ndani ya magari manne ya kukodi kuelekea Igunga.
Tukio hilo lilitokea jana saa 10:00 alfajiri katika kizuizi cha magari cha Tinde- Shinyanga baada ya CCM kupata taarifa kwamba vijana hao walikuwa katika mabasi hayo ya kukodi wakiwa na mapanga kwa ajili ya kufanya fujo katika uchaguzi.
Baada ya kupata taarifa hizo, January akiwa viongozi wengine, Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Benno Malisa, Mjumbe wa Kamati Kuu ya UVCCM, Hussein Bashe na Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Khalfan Aeshi, waliongoza vijana wenzao wa Green Guard na kuzingira magari hayo.
Mabasi hayo yalisimama katika kizuizi hicho cha polisi saa 7:00 usiku wakisubiri kupambazuke kutokana na sheria kutoruhusu mabasi kusafiri usiku.
Msafara wa magari saba wa CCM uliondoka Igunga saa 9:00 usiku kuelekea kwenye kizuizi hicho cha Tinde lakini kabla ya kufika, waliona gari la polisi likiwa limeegeshwa umbali wa mita 200 kutoka katika kizuizi hicho wakasimama na kujitambulisha.
Kutokana na unyeti wa tukio hilo na sababu za kiusalama, polisi waliwashauri viongozi hao wa CCM wasiende katika eneo hilo hadi kupambazuke na wakati huo polisi nao wakiongeza nguvu.
Kulipoanza kupambazuka, vijana hao wa Chadema wakiwamo wasichana wawili waligundua kuwa wamezingirwa na kuamua kushuka katika mabasi hayo.
Vijana wa CCM waliwadhibiti na walipowahoji walikiri kuwa wao ni wafuasi wa Chadema na wanakwenda Igunga kama mawakala wa chama hicho na si vinginevyo.
Hali katika eneo hilo ilizidi kuwa tete ilipotimu saa 1:00 asubuhi baada ya vijana hao kusikika wakiwasiliana na viongozi wa Chadema Igunga na kuwajulisha kuwa wamezingirwa na vijana hao wa CCM.
Ili kuepusha vurugu, polisi waliamua kuwarudisha vijana hao kwenye mabasi waliyokuwamo na kufanya upekuzi. Taarifa zilizopatikana baadaye jana zilisema kuwa hawakukutwa na silaha yoyote kama ilivyokuwa ikidaiwa na CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo hilo, kiongozi wa kundi hilo, Devota Ngaiza alisema: “Sisi hatuendi kufanya vurugu wala kupiga kura. Tunakwenda kukiongezea chama chetu nguvu wakati tunaelekea kipindi cha lala salama na tunawahakikishia tutabadilisha upepo.”
Devota alisema kitendo cha viongozi wa CCM akiwamo Makamba ambaye walisema walimtambua bila shaka yoyote, kinadhihirisha kuwa unyanyasaji waliofanyiwa na polisi ikiwamo kupekuliwa ulikuwa ni maelekezo ya CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Malisa alisema idadi ya vijana wanaoingizwa na Chadema Igunga wanatishia amani ya jimbo hilo kwa kuwa haifahamiki wanakwenda kufanya kazi gani hasa.
“Nataka niwahakikishie Chadema na umma wa Watanzania kuwa tunaifahamu mipango yote ya Chadema na UVCCM tumejipanga na tunasema tunao uwezo wa kuwadhibiti vijana wa Chadema,” alisema.
Kwa upande wake, Makamba alisema CCM hakina shaka ya ushindi kwani mtaji wake upo kwa makundi ya wanawake na watu wazima... “Wapiga kura wetu ni wale wanaopenda amani ambao ni kina mama na watu wazima, wenzetu wanalijua hilo kuwa nguvu ya CCM iko kwa kina mama na watu wazima.”
Alisema chama chake kinaamini kwamba endapo uchaguzi huo utafanyika kwa amani, usalama na bila vitisho kitashinda.
Awali, Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli alidai kuwa chama hicho pinzani kiliingiza vijana 600 jimboni humo na wengine 600 walitarajiwa kuingia kati ya jana na leo akidai kuwa kinajenga mazingira ya vurugu... “Mawakala wa Chadema na CCM, waliapishwa wote Septemba 27, sasa wanaoletwa watakuwaje mawakala wakati hawajaapishwa?”
Makamba aliitaka NEC ijiridhishe kuwa mawakala watakao kuwa vituoni ni wale walioteuliwa na vyama vyao na kuapishwa.
Chadema yabeza
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema CCM wameingiwa na hofu ya kushindwa uchaguzi huo.
“Hizo ni panic (hofu) zao kwa sababu maji yako shingoni na tunachokiona sasa upo mkakati wa CCM kushirikiana na jeshi la polisi kuwatisha vijana wetu waliojitolea kuja Igunga kushiriki operesheni za Chadema,” alidai.
“Ni kweli tunao vijana na viongozi wanakuja kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na wala si siri na walizuia kundi linalotoka Singida pia na wakazuia kundi jingine linalotoka Moshi na Arusha lakini nguvu ya umma itashinda.”
Alisema makundi ya vijana yaliyozuiwa katika maeneo ya Babati, Singida na Shinyanga ni zaidi ya 200 na kwamba matukio hayo yalitokea usiku wa kuamkia jana.
“Wamewapekua na hawajawakuta na silaha yoyote ni hofu tu ya CCM kwani wao wameleta watu wangapi hapa Igunga?”
Katika siku za hivi karibuni, CCM na Chadema zimekuwa zikituhumiana kila kimoja kupanga njama za vurugu kwa kuingiza vijana mamluki wenye mafunzo na silaha za jadi na za moto jimboni hapa.
Shutuma za CUF zaelekezwa NEC
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Ismail Jussa alidai kwamba kuna zaidi ya majina 3,000 ambayo hayaonekani katika orodha ya wapiga kura iliyobandikwa katika vituo 427 jimboni hapa.
Jussa alisema mbali ya majina hayo kukosekana, wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa watu ambao wana vitambulisho vya kupigia kura lakini hawakuona majina yao katika orodha hiyo.
“Tunashangazwa na tabia hii ya Tume ya Uchaguzi ambayo imekuwa ikijitokeza katika chaguzi kuu ili kuisaidia CCM kushinda inajitokeza tena katika uchaguzi huu mdogo wa Igunga,” alisema Jussa.
Alisema inashangaza kuona NEC inashindwa kuandaa uchaguzi huo bila kuwa na makosa... “Tafsiri yetu katika hili ni kwamba NEC inaandaa mazingira ya kuipa CCM ushindi.”
Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa muda wa Nec Profesa Amon Chaliga, alisema Tume yake haijapokea malalamiko yoyote kuhusu watu ambao hawakuona majina yao katika orodha.
“Tumekuwapo hapa na jana nilikuwa na mkutano na viongozi wa vyama vya siasa, walieleza mengi lakini hilo mnalolisema hawakusema, hata hapa hatujapokea rasmi taarifa hizo,” alisema Chaliga na kuongeza:
“Kama kweli kuna matatizo basi watuletee majina hayo maana hapa tuna wataalamu wa masuala ya kompyuta wa Tume na wanaweza kurekebisha kila kitu hapahapa na hao wanaodaiwa kutokuona majina yao wakapiga kura.”
Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Igunga, Protas Magayane alisema majina yaliyoripotiwa kuwa na matatizo wakati wa uhakiki ni 22 tu na kwamba matatizo yao yameshatatuliwa.
Nahodha, RC, DC lawamani
Katika hatua nyingine baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamekosoa hatua ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwasa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatma Kimario kuonekana wakiingia katika makazi ya muda ya CCM.
Viongozi hao wamekitafsiri kitendo hicho kuwa ni ishara ya Serikali kukisaidia CCM na kwamba kufika kwao katika makazi hayo yaliyopo katika Hoteli ya Peak ni kwa ajili ya kupanga mikakati ya ushindi ya chama hicho.
Juzi asubuhi viongozi hao walionekana wakiingia katika hoteli hiyo walipo viongozi wa CCM wakiongozwa na Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama na kukaa kwa muda kabla ya kuondoka.
CCM kwafukuta
Kitendo cha January na Aeshi pamoja na makada wengine vijana wa CCM kwenda ofisi za Chadema kimechafua hali ya hewa ndani ya chama hicho hapa ikielezwa kwamba kitendo hicho hakikuwa na baraka za chama.
Katika tukio hilo, wafuasi wa Chadema walimteka kwa muda Aeshi wakimtuhumu kukichafua chama chao. Inadaiwa kuwa pamoja na nia nzuri ya viongozi hao vijana wa CCM, yaliyojitokeza hapo yalizidi kuchafua upepo wa chama hicho.
Matokeo ndani ya saa 24
Kwa upande wake, NEC imesema itafanya kila linalowezekana kukata mzizi wa fitina kwa kumtangaza mshindi usiku wa kuamkia Jumatatu, Oktoba 3, mwaka huu.Profesa Chaliga alisema hatua hiyo inalenga kuepusha vurugu au kuwapo kwa vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo husababishwa na matokeo kuchelewa kutangazwa.
Profesa Chaliga aliwaambia waandishi wa habari kwamba ikiwa hakutakuwa na mvutano katika chumba cha kujumlishia kura, hakutakuwa na sababu za kuchelewa kutangaza matokeo.
“Tunaamini kwamba kila kitu kitakwenda sawa na kama hivyo ndivyo, basi hakutakuwa na sababu ya kuchelewesha kutangaza matokeo... na kila uchaguzi mdogo uliofanyika, imethibitika kwamba matokeo yanaweza kutangazwa mapema,” alisema.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Magayane ambaye alisema: “Tutajitahidi na ikiwezekana tutangaze matokeo ya uchaguzi usiku huohuo.”
Wizi wa kura
Akizungumzia madai ya wizi wa kura, Profesa Chaliga alisema mfumo wa usambazaji wa vifaa, upigaji kura, kuhesabu na hata kujumlisha hauruhusu wizi wa kura, isipokuwa tu kama mawakala wa vyama vya siasa hawatafanya kazi zao ipasavyo.
"Hawa mawakala wana wajibu wa kulinda maslahi ya vyama vyao na wagombea wanaowawakilisha, hawa wanashiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi, lazima wafanye hivyo ili kuhakikisha kwamba taratibu zinafuatwa,” alisema Profesa Chaliga.
Kuhusu madai yaliyotolewa na Mbowe kwamba kuna masanduku ya kura bandia ambayo yamefichwa katika moja ya nyumba mjini Nzega, Profesa Chaliga alisema NEC haijapata taarifa.
Alisema masanduku hayo kama yapo hayawezi kupata fursa ya kuingizwa kwenye mfumo rasmi wa upigaji kura isipokuwa tu ikiwa mawakala wa vyama, polisi na wasimamizi wa uchaguzi watakubaliana kwa umoja wao kukiuka sheria na kuruhusu hali hiyo.
“Sasa hapo ndipo nasema kwamba mawakala na polisi wanatakiwa wafanye kazi yao, masanduku ya kura yanapokusanywa yanasindikizwa na mawakala wa vyama wanaokuwa katika vituo ukusanyaji wa masanduku unapoanzia, sasa kama hawawezi kutekeleza wajibu wao, basi hayo yanaweza kutokea, lakini mfumo wetu ni imara,” alisema Profesa Chaliga.
Habari hii imeandikwa na Neville Meena,
Daniel Mjema na Godfrey Nyang'oro, Igunga.